Twitter

Twitter Buttons

Friday, 27 September 2013

Mwinyi Kazimoto na Ubora Wa Ligi ya Timu Sita Huko Qatar


Kazimoto ndani ya Jezi ya Al Markhiya
Licha ya kuwa wanasoka wa Tanzania wamekuwa wazito kuvuka mipaka kucheza soka la kulipwa, hali ni tofauti unapoongelea Uarabuni. Ni kweli kuwa milango ya kucheza soka la kulipwa bado ni migumu kufunguka jambo lilojidhibitisha kwa mara nyingine msimu huu ambapo ni wachezaji wawili tu, Kapombe na Kazimoto walioweza kuvuka mipaka baada ya kumalizika kwa ligi kuu. Hata katika uhamisho wa wachezaji hao wa Simba jambo lilojidhihirisha ni ugumu wa uuzwaji wa wachezaji wetu. Kwa lugha nyepesi ambayo hata wakala aliyesimamia uhamisho wa Kapombe alikiri na kuitumia ni kuwa ' wachezaji wetu bado ni bidhaa isiyouzika kimataifa'.

Ugumu wa uhamisho wa Kapombe unajulikana kwa wote wanaofuatila kandanda la nchi hii na kama si jicho zuri la biashara na akili za kujiongezea kutoka kwa wakala wake pamoja na viongozi wa Simba hakuna shaka chipukizi huyo ilikuwa arudi kwenye mpira wa Temeke. Bidhaa yetu, yaani wachezaji wetu bado ni bidhaa isiyo na thamani kwenye soka la kimataifa. Hata ligi ya Afrika Kusini ni ngumu kwetu.

Nirudi kwenye suala la Kazimoto, kiungo wa timu ya taifa ambaye wengi tunaamini ni moja ya viungo waliobarikiwa vipaji vya hali ya juu. Licha ya kipaji chake na umahiri alionesha uwanjani katika jezi za Simba na Taifa Stars ukweli unabaki kuwa Kazimoto hakufanikiwa kupata timu ya ligi kuu Qatar. Hakufanikiwa kuvishawishi vilabu vya ligi kuu Qatar na kuangukia ligi ya pili yenye timu sita tu. Ndio, timu sita! Wakati nchini tunalia kuwa udhaifu wa ligi yetu unachangiwa na uchache wa vilabu, Kazimoto yupo kwenye ligi ya timu sita. Tujiulize amepiga hatua, ameganda au amerudi nyuma?

Kiuchumi, yaani maslahi yake binafsi hakuna shaka kuwa amepiga hatua. Bila shaka anaweka kibindoni kitita kikubwa zaidi ya kile alichokuwa anapata Msimbazi. Kutoka JKT Ruvu kwenye mshahara wa laki na sabini, kujaa Simba hadi Qatar ni hatua kubwa kiuchumi. Inawezekana hakuna sifuri iliyoongezeka kwenye mshahara wake lakini ni lazima kuna namba kubwa zimeongezeka,hilo halina shaka hasa kwa nchi yenye uchumi mzuri kama Qatar.

Hata Simba, licha ya usiri na mkanganyo ( Bonyeza Hapa kusoma Makala inayochambua mkanganyo wa malipo ya Uhamisho wa Kazimoto) kwenye malipo bado wamefaidika kiuchumi. Bingwa wa ligi nchini anapewa takriban dola elfu hamsini ambazo zinakaribiana na kiasi walichopokea Simba kwenye uhamisho wa Kazimoto. Yaani ni sawa na kusema hata Simba wakikosa ubingwa msimu huu ni kama wameshapata zawadi ya ubingwa kutokana na mauzo ya Kazimoto. Kiuchumi ni bao zuri kwa Simba na Kazimoto, wote wamefanya biashara.

Swala la maendeleo binafsi na mchango kwa taifa wa mchezaji wa kulipwa Uarabuni ni tata kidogo na wengi tutatofautiana, wengine tutasema ni hatua mbele ilhali wengine watasisitiza ni hatua kurudi nyuma. Pia kuna wachache wanaweza kuwa wanaamini hakuna hatua aliyopiga, yaani kiushindani wa ligi yupo pale pale.

Kutokana na viwango vya wachezaji wengi kuonekana kuporomoka baada ya kwenda Uarabuni kuna kasumba iliyojengeka kuwa ligi za Uarabuni ni dhaifu. Tena hoja ya udhaifu huo inapigwa jeki na wingi wa Wachezaji wa Tanzania waliopata fursa ya kucheza Uarabuni kulinganisha na mabara mengine. Kauli za kuwa hakuna anayeshindwa majaribio ligi za Uarabuni zinaipa nguvu zaidi hoja ya kuwa ligi yetu ni bora kuliko ligi nyingi za Uarabuni.

Nakumbuka kauli ya kocha wa zamani wa Yanga, mkongomani Raul Shungu baada ya kumtazama Waziri Mahadhi aliporejea nchini kutoka Uarabuni. Shungu alitikisa kichwa kama vile aamini kisha akatamka ' Mahadhi amenepa hadi kichwa! Mpira wote umepotea miguuni..."  Waziri Mahadhi aliyerudi nchini si yule aliyeondoka huku akiwaacha mashabiki na kumbukumbu za Mendita  hasa kwa soka alilopiga kwenye michuano ya Castle Cup...walioangalia mechi ya Taifa Stars dhidi ya Simba wa Kongo  kwenye Castle Cup pale Arusha watakuwa wana kumbukumbu nzuri. Waziri Mahadhi ni mfano mmoja kati ya mingi ya wachezaji waliotimkia Uarabuni na kurejea makapi. Hata Ghana wanalia na Asamoah Gyan kukimbilia Uarabuni licha kuwa huwezi kulinganisha ligi  aliyotoka Gyan na aliyotoka Kazimoto.

Kazimoto yupo kwenye ligi ya timu sita tena si ligi kuu, tujiulize kapiga hatua mbele kiuchezaji au ni hatua kurudi nyuma? Ligi ya daraja la pili Qatar ni bora kuliko ya kwetu? Nizar Khalfan na Danny Mrwanda baada ya kwenda Kuwait walirudi vipi? Je, ni kweli Nizar aliyetoka Kuwait si yule aliyekuwa hapa akiwatungua makipa kwa mikwaju ya masafa marefu? Kazimoto aliyeondoka nchini akipiga pasi za uhakika atarudi vipi? Ligi yenye pesa lakini ushindani wa timu sita tu utamkuza au kumshusha kiwango? Yaani msimu mzima kama asipokaa benchi na kuepuka majeruhi Kazimoto atacheza mechi 11 za ligi.

Pia tusisahau, kitakwimu ligi kuu ya Qatar iko juu yetu. Ina makocha wa kimataifa haswa, wakufunzi waliodhibisha ubora wao kwenye dunia ya Kwanza kisoka na kiuchumi.  Hakuna shana kuwa Qatar wanatuzidi vitu vitatu kati ya vinne vinavyotakiwa kukatika ukuzaji wa soka, ubora wa vifaa,walimu, na viwanja. Naamini kuwa tunawazidi jambo la nne, yaani vipaji. Mtu akikuzidi kwenye vitu vitatu na wewe ukamzidi kimoja mnaweza kulingana? Wenzetu wana vifaa bora, viwanja safi na walimu bora tunaweza kuwazidi kweli? Kipaji ni sehemu ndogo tu ya mchezaji, wengine wamediriki kusema ni aslimia 10% tu ya mchezaji bora. Tutawezaje kusema ligi yetu ni bora kwa misingi ya vipaji tu?
 (Pia Soma makala inayohusiana na hii Kazimoto Transfer Fee: Is it a back-door Deal? )


No comments:

Post a Comment