Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ziko nyuma sana
katika michezo, pengine kuliko ukanda mwingine wowote hapa Afrika.
Ukilinganisha na majirani nchi jirani, hali ni mbaya
zaidi kwa Tanzania. Hili utaligundua kwenye mashindano ya ndani ambayo
hayahusishi timu za taifa, mfano mashindano ya vyuo vikuu na shule za
sekondari.
Miaka yote tumekuwa tukilalamikia maandalizi duni na
visingizio vya kufanana na hivyo lakini ukitazama jinsi nchi kama Kenya na
Uganda zinavyotia mkazo michezo mashuleni ni wazi kuwa tunastahili matokeo
tunayoyapata.
Mara kadhaa nguvu za serikali na wadau zimekuwa katika
timu chache za taifa, hasa soka na kuitenga michezo mingine. Hata bajeti ya
Wizara husika hujikuta ikitumika sana kuhudumia soka kuliko michezo mingine.
Pamoja na ukweli kuwa kuboresha michezo kunahitaji
fedha na mipango ya muda mrefu, kuna baadhi ya nchi zina nafasi ya kufanya
vizuri kuliko zingine kutokana na sababu za kimazingira.
Tunaweza kujiuliza kwanini Kenya na Ethiopia hufanya
vizuri kwenye mbio ndefu kuliko mataifa mengine? Si kwamba Kenya wamewekeza sana kwenye riadha
kuliko mataifa ya Ulaya, lakini mahali walipo na aina ya watu walionao
kunawawezesha kufanya hivi.
Inaweza kuchukuliwa kama mtazamo wa kikabila, lakini
ukweli ni kuwa wanariadha wanaofanya vizuri kutoka Kenya huwa ni wa makabila fulani
tu, hasa jamii za Kifugaji za Nandi, Kalenjen na Maasai.
Isaiah Kiplagat, Peter Cheruiyot, Pamela Jelimo, Vivian
Cheruiyot na Prisca Cherono ni miongoni mwa wanariadha mahiri ambao wanatoka
katika jamii za wafugaji.
Utafiti uliofanywa na Scott na wenzake miaka ya 2005 na
2009 nchini Ethiopia na Kenya ulibaini kuwa watu wa jamii za eneo la Arsi,
Ethipia na Mlima Kenya wana vinasaba ambavyo vinawawezesha kuwa wakimbiaji
mahiri wa mbio ndefu. Inashangaza kuona eneo ambalo wakazi wake hawafiki
asilimia 0.1 ya wakazi wa dunia kuwa na medali zaidi ya 50 za michezo ya
Olimpiki.
Tafiti fulani za mwaka 2007 huko Kenya zilidai kuwa jamii za Kifugaji hutoa wakimbiaji
mahiri kutokana na matumizi makubwa ya maziwa ya ng’ombe.
Majibu tafiti hizi yanaweza yasiwe sahihi kwa asilimia
zote lakini hata ukitazama nchini kwetu, wakimbiaji mahiri walioipa sifa nchi
hii kama Filbert Bayi, Francis Naali na Wilhelm Gidabuday wanatoka kwenye jamii
hizi hizi za kifugaji.
Kukimbia riadha kwa vijana wadogo wa jamii za hizi za
Kaskazini, sio tu mchezo wa mashindano, lakini pia ni hulka na mchezo wa
kujifurahisha, kama vile soka ilivy katika jamii nyingi.
Laiti kama Chama cha Riadha (AT) kingeelekeza nguvu
nyingi katika kuboresha mazingira ya riadha kwa chipukizi wa jamii za wafugaji pengine
tungekuwa na medali nyingi zaidi za riadha katika mashindano kama vile IAAF,
Diamond League, Olimpiki na mengineyo.
Mchezo wa kuogelea ni moja ya michezo ambayo tunaweza
kunufaika nayo. Hapa tulipo tayari tuna
waogeleaji ambao hawakupita shule yoyote ya michezo lakini tayari ni mahiri.
Wengi wao hutoka visiwani kama vile
Zanzibar, Ukerewe, Mafia na sehemu za pwani kama Dar es Salaam na kadhalika.
Kama ukibahatika kutembelea ufukwe wa Coco siku za
wikiendi, wapo vijana ambao hucheza mchezo wa kujirusha kwenye maji kwa
kujifurahisha tu. Kama mtu anaweza kucheza mchezo kwa kujifurahisha, kwanini
asitengenezewe mazingira mchezo huo ukampa faida?
Mara nyingi tumehangaika kuwapa hamasa wachezaji wetu
wanapocheza mashindano ya kimataifa, hatuoni kwamba tukiwa na wachezaji wa aina
hii tayari ni hamasa tosha?
Pengine Chama cha Kuogelea (kama kipo) hakijafanya
tafiti kujua wapi hasa tuweke msisitizo katika kukuza vipaji vya waogeleaji. Si
kila shule inaweza kufundisha kuogelea na kukawa na mafanikio. Mahali ambapo
maji ya kunywa hufuatwa kilomita tano huwezi kupata waogeleaji kwa namna
yoyote.
Mbio za baiskeli ni mchezo mwingine ambao tunaweza
kufanya vizuri kama tutaamua kuchanga karata zetu vizuri. Wakazi wa kanda ya
ziwa ni waendeshaji mahiri wa baiskeli na hata vijana wamejiajiri katika sekta
ya usafirishaji kwa kutumia njia ya baiskeli.
Mara kadhaa tumeshuhudia mikoa ya Mwanza na Shinyanga
wakiwa wenyeji wa mbio za Baiskeli lakini sina hakika kama tulishawahi
kufikiria kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kidunia kama Tour de France.
Kwa jicho jepesi, naona tunao uwezo wa kushiriki
mashindano haya bila kikwazo chochote. Wasafirishaji wa abiria kwa njia ya
baiskeli huweza kumbeba mtu mwenye uzito wa kilo 70 au 80 kwa umbali wa kilomita
kadhaa. Ni wazimu kudhani kuwa hawataweza kushindana na waendeshaji wa
kimataifa ambao hutumia baiskeli nyepesi zisizo na mzigo wowote.
Hapa tunahitaji mafunzo machache tu ya kuwawezesha
vijana hawa kuendesha baiskeli kwa viwango vya kimataifa na miaka kadhaa mbele
tutakuwa na wawakilishi katika Tour de France.
Michezo ni ajira na sehemu ya kukuza uchumi, kama
nafasi ipo ya kufanya vijana wetu wanufaike na michezo wanayoiweza tufungue
macho. Tusiishie kufundisha michezo ile ile kwenye mitalaa yetu miaka nenda
rudi. Vipaumbele vya vyama vya michezo na Baraza la Michezo vizingatie ufanisi
wa maeneo husika katika michezo wanayoisimamia.
Nchi kadhaa duniani zimeshajipambanua na kuweka nguvu
zao katika michezo wanayoiweza hata kama haina mashabiki wa kutosha kama ilivyo
mingine. Ni wakati wa sisi kutazama kipi tunakiweza zaidi na tuwekeze huko kwa
nguvu zote.
Mwandishi: Mphamvu Daniel
Simu; 0717474832
Barua pepe; mphamvu@facebook.com
No comments:
Post a Comment