Twitter

Twitter Buttons

Wednesday 14 August 2013

Michezo Inahitaji Wanaharakati Kubadili mfumo mbovu uliopo



Harakati si jambo geni miongoni mwa waTanzania. Yapo makundi ambayo yamejipambanua kama makundi ya wanaharakati. Wapo wanaharakati wa mambo ya siasa, haki za binadamu, mazingira na kadhalika.
Hawa kazi yao ni kusimamia au kuangalia endapo mambo katika sekta wanayoisimamia yanaenda kama inavyotakiwa. Wanaharakati wa mazingira kwa mfano, wapo kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa sheria na sera za mazingira katika ngazi za kanda na kitaifa.

Kwa muda mrefu, sekta ya michezo imeachwa kama sekta inayojiendea yenyewe tu. Ikiwa na wateule wachache ambao wamo ndani ya mfumo teule waliojiamulia.
Mara nyingi umesikia kuwa chama cha mchezo fulani kina wenyewe, au ukitaka kuingia Yanga au Simba lazima ujuane na fulani.
Kuachwa kwa hali hii ya kuwa bila uangalizi pengine ni moja ya sababu ambazo zinafifiza michezo nchini. Kama ndivyo, hakika tunahitaji watu ambao wataitazama sekta ya michezo kwa jicho huru, ukipenda waweza kuwaita wanaharakati.

Mchezo kama soka, umesuswa na wadau wenye mawazo chanya kwa kuwa washabiki wana mbadala katika kukidhi kiu yao ya mpira.
Ndio, watu wameshaamua kushabikia ligi, timu na mechi za Ulaya kweupe tena kwa kujivuna. Si ajabu kusikia mtu akidai kuwa yeye ni Manchester ‘damu’, au Barcelona na timu nyingine kubwa za Ulaya.
Kwa minajili hii, wadau hawa hawaoni haja ya kuwa sehemu ya mabadiliko katika sekta ya michezo nchini. Wamesharidhika na kuwa washabiki wa kufikirika wa Rafael Nadal, Arsenal, Chelsea, Usain Bolt, timu ya taifa ya Hispania na kadhalika. Mara kadhaa tumewasikia wachambuzi wa michezo wakitoa chambuzi murua kabisa kuhusu michezo ya Ulaya, chambuzi ambazo kwa vyovyote hazina manufaa kwetu na hao wanaowachambua hawatazisikia kamwe.

Laiti nguvu hii ingetumika katika kurekebisha michezo yetu inayoyumba, pengine tusingekuwa na medali mbili tu katika michezo ya Olimpiki. Ni rahisi kukuta mtu mzima katika viunga vya mji wa Dar es Salaa akilalamika kwa hisia kabisa kuwa Arsene Wenger anawaharibia timu yao (akimaanisha Arsenal) au kuwakuta washabiki wakiulizana kwanini timu yenu haisajili wachezaji?
Si rahisi kuthibitisha kuwa katika michezo kuna ufisadi lakini matukio kadhaa yanaashiria uwepo wa rushwa michezoni. Wakati fulani, mwanariadha mstaafu, Wilhelm Gidabuday alijitokeza wazi kueleza mapungufu ya Kamati ya Olimpiki (TOC) na ubadhilifu wa mwenyekiti wake, Filbert Bayi. Majibu ambayo Bayi aliyatoa kwa kituo kimoja cha redio, yalionyesha wazi kuwa kilichosemwa na Gidabuday kumhusu kina mantiki ndani yake.

Wanaharakati kama Gidabuday, ambao wamejitahidi kuanika  mapungufu ya taasisi zetu za michezo wamekuwa wakikabiliwa na uungwaji mkono usioridhisha kutoka kwa jamii. Pengine tofauti na wanaharakati wa siasa ambao jamii huwaunga mkono katika kila hatua wanayopiga.
Mapema mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu liliahirisha uchaguzi wake mara kadhaa kwa madai ya kukosa fedha za kuendesha uchaguzi huo. Pamoja na TFF kuwa na mikataba na TBL na NMB, na fedha za miradi ya Goal!, malaria na fungu ambalo hutoka FIFA kila mwaka, bado viongozi wa TFF walipata ujasiri wa kusema kuwa hakuna fedha za uchaguzi. Haihitaji kuwa na elimu ya chuo kikuu kujua kuwa huu ni ufisadi wa mchana kweupe, bado wadau wa soka wakaliacha hili lipite hivi hivi.

Zaidi ya hayo, vyama na taasisi za  michezo zimekuwa ni sehemu za watu kufanya biashara haramu na kufanya uhalifu. Kesi ya kusafirisha madawa ya kulevya iliyowakabili mabondia wa timu ya ridhaa ni ushahidi tosha kuwa watu wanatumia taasisi hizi kwa manufaa yao binafsi. Wanasiasa ambao wana kesi za jinai za ufisadi wamekuwa wakijificha kwenye kivuli cha vyama vya michezo. Kwa hali hii ni wazi kuwa tunahitaji watu wa kuyakemea haya kwa sauti kubwa kama ambavyo kuna watu wa kukemea maovu katika siasa na kwingineko.

Vyama vya soka vimekuwa sehemu ya kukimbilia kwa wanasiasa ambao wanasaka umaarufu kwenye medani yao. Wabunge na mawaziri kadhaa pia ni wanachama hai na viongozi katika timu mbalimbali za soka. Hili si jambo baya, lakini ni wazi kuwa michezo imetumika kama sehemu ya kusaka umaarufu ili watu wakawe wabunge na mawaziri. Kwa hali ilivyo, hatuhitaji watu ambao watakuwa wanatumia vyama na timu za michezo kwa ajili ya kupata umaarufu na kisha kutokomea.

Hali ya sekta ya michezo kukosa watu wa kuisemea imepelekea kudumaa kwa vipaji vingi. Vyama vya michezo vimekuwa vikiendeshwa kwa mazoea na viongozi wamefika hatua ya kuviona kama mali yao binafsi.
Tunahitaji watu wa kuyasema haya hadharani na kuyakemea. Awali, nilitegemea sana sauti za vyombo vya habari lakini ni wazi kuwa vyombo hivi haviwezi tena kuwa sauti dhidi ya ubadilifu michezoni. Waandishi wa habari wamekuwa viongozi wa michezo, au la wamekuwa wakishirikiana na viongozi hawa katika harakati zao.

Laiti tukipata watu wa kuiambia jamii maovu ya viongozi wa michezo, pengine hali itabadilika au watang’oka madarakani na kuwapisha wenye nia ya kuendeleza michezo.


Mwandishi: Mphamvu Daniel
Simu; +255717474832
Barua pepe; mphamvu@facebook.com

No comments:

Post a Comment