Licha ya uwekezaji wa kiwango kikubwa , ubingwa wa ligi kuu
umeendelea kuwa simulizi ya ‘msimu ujao’ kwa vijana wa Chamazi. Kwa misimu
miwili mfululizo, wamekaribia sana kutwaa ubingwa lakini mara zote wamefia
ufuoni na kuwaacha wakongwe Simba na Yanga wakishangilia. Kwenye msimu huu
mpya, Kwa mara nyingine watajitupa kwenye ulingo kupigania ubingwa wa ligi kuu.
Licha ya kushiriki michuano ya Afrika, akili na nguvu zao zitakuwa zimeelekezwakwenye ligi kuu kuhakikisha wanapambana mpaka dakika ya mwisho kuchukua ubingwa. Ndio kombe la msingi zaidi kwao
licha ya kuwa kombe la shirikisho ni kubwa zaidi. Kombe la shirikisho litabaki
kuwa mazoezi ya ndoto zao za siku za usoni.
Azam,licha ya kuhesabika kama moja ya vigogo vya soka
nchini, bado hawajaingia rasmi katika historia ya vigogo wa soka nchini. Ubavu
wao wa fedha unaweza kuwa umewapa heshima ya kuitwa vigogo lakini kihistoria
wao bado ni kinda kwa Coastal Union, Mtibwa Sugar na Pamba . Hivi ni baadhi tu ya
vilabu ambavyo vipo katika kumbukumbu za historia za ubingwa Tanzania. Kwa sasa
Azam ni vigogo lakini ni kofia ya ubingwa tu ndio itawapa heshima na hadhi ya
kuitwa vigogo wa soka nchini. Jeuri ya pesa inaipa klabu ukuu wa muda tu,
ubingwa unatoa hadhi ya kihistoria. Mwisho wa siku, historia huandikwa na
mabingwa tu.
Azam waliingia kambini mapema, wamefanya ziara ya siku kumi huko
Afrika Kusini Pamoja na mikakati mingine katika jitihada zao za kujifua kwa
ajili ya mbio za ubingwa wa ligi kuu. Licha ya yote hayo,kamari kubwa zaidi
waliyocheza ni kutosajili wachezaji wapya kwa msimu huu. Ni ngumu kuamini
kuwa ni mkakati wa utawala kuamua
kutosajili hasa baada ya kukaribia sana kutwaa ubingwa msimu uliopita. Kwa
namna yoyote ile utakuwa ni uamuzi wa kocha wao.
Inawezekana kocha Stewart Hall ameamua kutengeneza mshikamano
na umoja katika kikosi kuliko kusajili wachezaji wapya ambao watachukua muda
kuelewana. Ameamua kuwafyeka baadhi ya wachezaji ambao ameona hatawahitaji na
kupandisha chipukizi kadhaa. Kati ya waliokumbwa na panga ni Pamoja na kiungo
mshambuliaji, Abdi Kassim, Abdulhalim Humud na kipa Munishi. Jambo la
kustaajibisha ni kuwa wawili kati ya watatu waliotemwa,Munishi na Humud
wameibukia kwa wapinzani wao wakubwa, Simba na Yanga. Kama filamu ya kejeli
hivi, Munishi katika mechi yake ya kwanza aliizuia Azam kuchukua ubingwa wa
kombe la ngao ya jamii kwa kuokoa hatari zote zilizoelekezwa langoni mwake.
Humud, kiungo matata, ambaye kama akitulia na kuamua kucheza
mpira Azam wanaweza kujikuta wakimwaga machozi kwa kuwapa silaha wapinzani wao.
Kwenye biashara za kuwania ubingwa ni kosa kubwa kumpa unafuu adui yako lakini
Azam ni kama wamefanya hivyo kwa kuwaimarisha Simba na Yanga. Suala la kutemwa kwa
Abdi Kassim lina utata zaidi hasa baada ya kila upande kutoa kauli tofauti. Kwa
waliofuatilia ligi msimu uliopita watagundua kuwa licha ya kuonekana kuwa umri
umemtupa mkono bado Babbi alitoa mchango mkubwa wa magoli.
Bila ya Abdi Kassim na huku Humphrey Mieno akiwa majeruhi,
Azam wanaweza kujikuta wakiwa hawana kiungo mshambuliaji wa kuwasidia ufungaji. Ukichungulia kwa wapinzani wao, Simba na Yanga utagundua wako
vyema kwa kuwa na Amri Kiemba na Haruna Niyonzima. Kuna wakati washambuliaji wa
Yanga walikuwa likizo ya kufunga lakini Niyonzima na Nizar Khalfan wakabeba
majukumu vizuri .Yanga ilijikuta ikiambulia ushindi wa bao moja mfululizo
kutokana na viungo washambuliaji kuwasaidia washambuliaji na hivyo kujikuta
timu ikisonga mbele bila kuyumba. Kwa upande wa Simba, mchango wa mabao wa Amri
Kiemba unajulikana.Kwa misimu miwili mfululizo sasa, Kiemba amekuwa msaada
mkubwa kwa Simba kutokana mabao anayofunga. Kwa jicho la haraka, utagundua Azam
hawana mtu wa hivyo msimu huu. Wamemtema Abdi Kassim na kushindwa kuziba pengo
lake.
Ni jambo la kusubiri na kuona mwisho wa msimu utakuaje licha
ya kuwa kuna dirisha dogo la usajili baada ya mzunguko wa kwanza. Stewart
anaweza kusajili kipindi hicho lakini kama watakuwa wamevurunda na kuachwa na
Simba au Yanga basi itabidi wasahau ubingwa kwa mara nyingine.Simba na Yanga
wakikutanguliza ni ngumu sana kuwakamata kwa kuwa mashabiki wao wanakuwa nyuma
yao kuwahamasisha. Kwa kucheza kamari ya kutosajili Stewart Hall anaweza
kuibuka shujaa au kuishia kufungasha virago na kurudi katika fukwe baridi za vya
Uingereza.
No comments:
Post a Comment