Msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu ya Vodacom ndio umeanza rasmi
kwa mechi za raundi ya kwanza kuchezwa mwisho wa juma. Mechi za kwanza
zimeshuhudia mabingwa watetezi , Yanga wakiibuka na ushindi mkubwa zaidi. Chini
ya kocha wao Mholanzi Ernie Brandts waliiporomoshea kipigo cha mbwa mwizi timu
ya Ashanti United iliyopanda daraja msimu huu.
Yanga ilitarajiwa kushinda lakini si kwa kutoa kipigo cha 5-1,
hili halikutarajiwa na wengi hasa ukizingatia kuwa Ashanti walionekana kuwa
wamejikakamua kwa maandalizi ya kutosha. Ashanti walipiga hatua hadi ya kufanya
ziara nje ya nchi katika kujiandaa na ligi. Wengi tulitarajia kuwa watatoa
ushindani kwa Yanga. Kinyume na matarajio wameambulia kipigo ambacho kinaweza
kuwa kipigo kikali zaidi katika msimu mzima.
Ingawa msimu ndio
umeanza, lakini Yanga wanaonekana kuwa kamili sana ukilinganisha na wapinzani
wao. Ukamili wa Yanga hautokani na kuwa na wachezaji bora kulinganisha na Simba
na Azam, la hasha, wapo bora kutokana na mbinu za kocha wao. Kwa mchezaji mmoja
mmoja, Simba na Azam wanaweza kuwa bora kuliko Yanga na pia wanaweza kuendelea
kutoa wachezaji wengi katika timu za taifa. Japo ni mapema sana lakini tunaweza
kushuhudia filamu ya msimu uliopita ya wachezaji wa Simba na Azam kutamba
katika timu ya taifa huku Yanga wakitesa kwenye mbio za ubingwa.
Ubora wa Yanga unatokana na mbinu za kocha wao kucheza
mchezo wa kushambulia moja kwa moja. Wako ‘direct’, wanatumia pasi chache
kulifikia lango la adui kulinganisha na wapinzani wao, Azam na Simba. Yanga
wana wachezaji wengi wenye kasi, kuanzia Msuva, Juma Abdul, Salum Telela hadi
ingizo jipya Mrisho Ngassa. Hawa ni hatari hasa wakikuta walinzi waliozubaa. Ni
tofauti na Azam na Simba ambao wanapendelea zaidi kumiliki mpira hasa kwenye
maeneo yasiyo na madhara kwa adui.
Ikumbukwe kuwa kocha Ernie Brandts alikuta ligi ya msimu
uliopita imekwishaaanza licha ya kuwa aliweza kubeba ubingwa. Msimu huu Yanga
inaweza kuwa hatari zaidi kwa kuwa kocha ameanza na timu toka mwanzo na hivyo
kupata muda mwafaka wa kushughulikia mapungufu.
Jambo la hatari zaidi kwa wapinzani wenye ndoto za kuwapokonya ubingwa Yanga ni
jeshi la mashabiki lililo nyuma ya Yanga hasa kwa kasi walioanza nayo. Hakuna
shaka kuwa Yanga inaongoza kuvutia mashabiki uwanjani na hasa timu yao
inapokuwa katika wimbi la ushindi basi mashabiki wake huongezeka maradufu.
Azam anaanzia ugenini mechi tatu za kwanza,ni ratiba ngumu
kwake. Ameanza kwa sare na Mtibwa Sugar kisha anamfuata Rhino Rangers kabla ya
kumalizana na Kagera Sugar huko Kaitaba. Simba naye anaanzia ugenini mechi
mbili za kwanza, ameanza kwa sare dhidi ya Rhino kasha anawafuata wanajeshi
wengine, JKT Oljoro kabla ya kupambana na Mtibwa Sugar nyumbani. Kwa haraka
haraka utaona kuna hatari ya Azam na Simba kujikuta wakiwa nyuma ya Yanga kwa
pointi kadhaa ndani ya raundi tatu tu za mwanzo. Yanga wao wanaanzia nyumbani
mechi mbili za kwanza,wamemsarambatuisha Ashanti, Coastal anawafuata kabla ya
wao kusafiri kwa kuku mgeni wa ligi, Mbeya City.
Simba na Azam itawabidi kuchanga karata zao vizuri ili
wasije kujikuta wanatimuliwa vumbi baada
ya raundi chache tu za mwanzoni. Yanga wakitoka, wapinzani wahesabu maumivu. Ni
hatari kuwaacha Yanga watangulie mbele, hasa Yanga hii chini ya mholanzi.
No comments:
Post a Comment