Twitter

Twitter Buttons

Thursday, 21 March 2013

Zali la Mentali kwa Taifa Stars



                                  ZALI LA MENTALI LINAWEZA KUTUANGUKIA TAIFA STARS
Ukichunguza vizuri  ratiba ya mechi za kuwania kufuzu kombe la dunia kwa bara la Afrika  utabaini mambo mawili.Mosi,hatua ya makundi ndiyo ngumu zaidi hasa kwa kuwa ni timu moja tu ndiyo itafuzu   kwa kila kundi.Kuna makundi kumi yenye timu nne.Hivyo basi timu kumi zitakazoongoza makundi yao zitafuzu kwa hatua ya mtoano ili kupata  timu tano zitakazowakilisha bara la Afrika kwenye kombe la dunia huko Brazil.
Hatua ya makundi ndiyo ngumu zaidi,kila timu itatakiwa kucheza mechi sita,tatu ugenini na tatu nyumbani. Kwa hesabu za haraka haraka mshindi wa kundi ni lazima ashinde mechi zote za nyumbani na angalau kushinda mechi moja au kutoa sare mbili ugenini.Kwa vyovote vile ushindi wa nyumbani ni lazima.Sare yoyote ya nyumbani ni kifo hasa ukizingatia kuwa ni timu moja tu ndiyo itakayofuzu kwa kila kundi. Tanzania tumeanza vyema kwa kuwafunga Gambia nyumbani,hatuna budi kuwafunga Simba wa milima ya Atlas kutoka Morocco ili kuendeleza ndoto zetu za kuisaka safari ya Brazil.

Pili,utababini kuwa hatua ya mwisho ni rahisi na imejaa bahati hasa kwa timu changa kama Tanzania.Hatua ya pili ni mechi mbili tu zinakuvusha hadi Brazil kula bata.Yaani unahitaji kuwa makini katika dakika 180 tu kuungana na wababe wengine Brazil. Ni rahisi kushinda nyumbani na kwenda kutafuta matokeo ugenini.Kwa mtindo huu Cape Verde walifuzu AFCON mbele ya wababe Cameroun. Cape Verde walimaliza biashara nyumbani kwa kushinda 2-0 kisha wakaenda kujitoa mhanga ugenini na kufungwa 2-1 na hivyo kuwatoa Cameroun.Zambia waliokuwa mabingwa watetezi almanusra wavuliwe ubingwa wao pale Kampala kabla ya kuponea chupu chupu kwenye matuta.Mtoano ni kamari nzuri kwa timu changa.Usishangae kuwaona vigogo Afrika wakizikosa fainali za kombe la dunia kwa mara nyingine  huku ‘watoto’ wakifuzu.

Kwenye kundi letu Ivory Coast ana nafasi kubwa  ya kufuzu licha ya kuwa ni mapema sana kutabiri. Ivory Coast wana silaha za kutosha kuziketeza timu nyumbani na ugenini.Historia yao ya hivi karibuni katika mechi za kufuzu inaonesha kuwa hawana shida kuzifunga timu ugenini. Kumbuka jinsi walivyowalambisha sakafu Senegal nyumbani na ugenini bila shida. Hawa wamekamilika.Hawa ndio tunaowahofia sana.

Morocco licha ya kushiriki kombe la Afrika huko Afrika Kusini na pia kutufunga nyumbani na ugenini katika mechi za kufuzu hawaonekani kuwa tishio sana.Morocco hawakuonesha lolote la kutisha huko Afrika Kusini,walitoa sare mechi zote.Pia hatuhitaji kwenda mbali sana kupata mfano kuwa wanafungika.Jirani zetu wa Rwanda waliwakimbiza sana na kuwapakata kwa kuwafunga 3-1 pale Kigali. Morocco pia wanaonekana kuwa na migogoro yao kuhusiana na wachezaji wao nyota.Kina Adel Taarabt, Chamakh na Hamdaoui wa Italia hawapo kwenye timu ya taifa kwa sasa.Kifupi hawa jamaa wanafungika.Pia sare pale Rabat au Casablanca inapatikana tukiwa makini.

Gambia hao licha ya kuwa Afrika Magharibi si timu ya kutisha,tuko katika kiwango  kimoja.Tumeshawafunga hapa,tunao uwezo wa kutoa nao sare au hata kuwafunga huko kwao.Kifupi  kama tukiwa makini tuna uhakika wa point inane bila kuweka mechi ya Ivory Coast.Kwa hivyo ni kuwa makini huku tukiomba Ivory Coast wajichanganye wenyewe.Kuteleza kwa Ivory Coast ndiyo zali letu la mentali.Kumbuka Ivory Coast wenye kawaida ya kushinda mechi zote wameisha toa sare moja,tumuombe Mungu waongoze sare nyingine na Gambia.Dua zetu japo ni za kuku zinaweza kuwapata…Soka halichezewi kanisani wala msikitini kwa hio maombi pembeni,maandalizi na mipango zaidi ili zali la mentali liwe ukweli na si wimbo tu wa Profesa Jay.

No comments:

Post a Comment