Macho na masikio ya wapenda kandanda nchini Kenya
yataelekezwa kwenye dimba la Nyayo mwishoni mwa juma hili. Pambano litakalovuta
hisia zote ni baina ya miamba wa Kenya, Gor Mahia itakayoluwa na kibarua kigumu
dhidi ya wajukuu wa Farao,ENPPI ya Misri. Gor Mahia ina kibarua cha kulipa
kisasi cha mabao 3-0 ili kuweza kupata nafasi ya kusonga mbele kwenye kombe la
shirikisho Afrika ngazi ya vilabu.
Kila masaa yanavyokatika ndivyo homa ya mpambano huu
inavyozidi kupanda hasa kwa maelfu ya wapenzi na wanazi wa Gor Mahia.
Kinachotia shaka si uwezo wa Gor Mahia bali ni ukubwa wa kipigo chenyewe.Ni
dhahiri kuwa kwa kuruhusu mabao matatu
kule Misri Gor Mahia ni kama walikubali kuingia kwenye mdomo wa mamba. Mabao
matatu ni mengi mno kwa timu yoyote ile.
Kazi iliyopo mbele si haba,inahitaji
mioyo ya chuma na roho za sabuni kukabiliana nayo.
Hata hivyo waswahili hunena mbwa hafi aonapo ufuo hasa
ikizangatiwa kuwa Gor Mahia watacheza mbele ya maelfu ya jeshi lao la mashabiki
watakaokuwa wakishangilia kwa mbwembwe zote. Itawabidi mashabiki wa Gor Mahia
kupasuka koo kwa kupaza sauti kuishangilia timu yao toka kipenga cha kwanza
hadi cha mwisho . Mashabiki watakuwa kama mchezaji wa kumi na mbili uwanjani katika kuhakikisha ushindi
unapatikana.
Licha ya kuwa Gor Mahia bado haijashika ule moto wake wa
msimu uliopita bado kuna matumaini makubwa hasa ukiangalia aina ya wachezaji
walio nao kikosini. Licha ya mkufunzi wao, Logarusic, kulililia kuwa majeruhi yamewaathiri sana bado
ana silaha zinazoweza kuiangamiza ENPPI kama akizumia ipasavyo.
Taratibu mshambuliaji hatari,Dan Sserenkuma anaanza
kurudisha makali yake ya msimu uliopita.
Pia mshambuliaji chipukizi aliyesajiliwa msimu huu kutoka KCB, Paul Kiongera
anazidi kuimarika kwa kuwaonesha mashabiki
thamani yake. Ikumbukwe Kiongera alianza kwa kusuasua kiasi cha kuzomewa
na baadhi ya mashabiki kwenyi mechi za awali. Wasi wasi unabakia kwa pacha wa
Sserenkuma,Rama Salim ambaye bado anaweweseka. Ushirikiano wa Rama Salim na Dan
Sserenkuma ulikuwa chachu kuu ya mafanikio ya Gor Mahia mwaka jana.
Safu ya ulinzi si mbaya,golini Jerim Onyango au Ivo Mapunda
wote wapo kamili,Donald Mosoti,David Owino aliyezima moto wa Victor Moses wa
Chelsea katika mechi dhidi ya Naijeria,Ivan Anguyo licha ya kuwa ameonesha
udhaifu pamoja na Wekesa wana uwezo wa
kuzima mashambulizi ya ENPPI.Kazi yao itakuwa kuhakikisha ENPPI hawapati bao lolote linaloweza kuharibu hesabu za Gor Mahia.
Safu ya Kiungo itakuwa na kazi ya kupika nafasi za mabao kwa
washambuliaji huku pia wakiipa kinga safu ya ulinzi dhidi ya mashambulizi ya
ENPPI.Bila shaka,Teddy Akumu,Ali Abondo,Njuguna na Kevin Abondo wataweza kuwapa raha mashabiki wa Gor Mahia na
kuhakikisha klabu ya Kenya inaonja ladha ya ushindi dhidi ya wamisri.
SOFAPAKA waliweza kuitoa Ismailia licha ya kufungwa 3-0
ugenini , ni jambo ambalo Gor Mahia pia wanaweza kulifanya.Uwezo wanao, sababu
za kufanya hivyo wanazo, na pia nia ya kufanikisha jambo hilo wanayo.Kila la
kheri Gor Mahia katika jitihada zenu za kujitoa kwenye kinywa cha mambo.
No comments:
Post a Comment