Twitter

Twitter Buttons

Thursday, 21 March 2013

HUKUMU YA KIFO KWA TUSKER

                                  HUKUMU YA KIFO KWA TUSKER
Vilabu vya Kenya vya Tusker na Gor Mahia vilijikuta vikiambulia vipigo kutoka mikononi mwa vilabu vya wajukuu wa Firauni.Tusker iliambulia aibu ya kuchapwa nyumbani na Al Ahly.Gor Mahia nayo ilisulubiwa na ENPPI kwa kubebeshwa furushi la mabao matatu bila jibu huko Misri. Ingawa wengi tuliona ugumu wa kupambana na vilabu vya Misri bado hatukutarajia kuona Tusker ikiaibishwa nyumbani au Gor Mahia ikibebeshwa furushi la mabao matatu na timu ya ENPPI hasa ukizingatia matatizo yaliyoikumbuka Misri baada ya machafuko ya kisiasa.
Kwa wale waliobahatika kuangalia mpambano wa Tusker na Al Ahly watakubaliana na mimi kuwa Al Ahly licha kutoonesha juhudi au maarifa ya hali juu bado walionekana kucheza kandanda la ufundi zaidi,akili zaidi na mipango zaidi. Hii ilikuwa ni Al Ahly dhaifu,bila ya kiungo wa mtaalam,Aboutrika na mshambuliaji mdokozi Gedo. Ilikuwa nafasi nzuri sana ya sisi kulipa kisasi cha kufungwa na Misri kila mara.Bahati mbaya tulishindwa kuitumia fursa hii. Wanaijeria huwa wanasema usipompiga mtu akiwa chini,je utampiga lini?
Tusker ina kibarua kigumu sana cha kupata matokeo mazuri huko ugenini.Timu za Misri hazipotezi mechi nyumbani.Licha ya kufuatila mashindano ya klabu bingwa Afrika kwa muda mrefu ni mara moja tu ndio nimebahatika kuiona klabu ya Misri ikipoteza mechi nyumbani.Mwaka jana,niliona Zamalek chovu ikilamba sakafu nyumbani mbele ya vijana hodari wa TP Mazembe. Wamisri wana viburi sana ,wana hulka ya kutumia kila mbinu kusaka ushindi nyumbani.
Itakuwa ngumu sana kupata nafasi za wazi kama zile tulizozipata hapa. Shikokoti,Dunga Jesse Were na chipukizi Olunga walishindwa kufunga mabao ya wazi kabisa ambayo ni wazi yangekuwa mtaji mzuri wa mabao kuelekea mechi ya marudiano huko Misri. Tusker walichezea shilingi yao chooni,huko Misri watarajie kuvuja jasho la damu na chumvi kuusaka mpira huku wakijitahidi kuzuia mvua ya mashambulizi kutoka kwa Al Ahly.
Licha ya kuruhusu mabao mawili,safu ya ulinzi ya Tusker ilikuwa likizo kwa muda mrefu kwani Al Ahly walikuwa wanauchezea mpira pembeni zaidi bila ya kuingia sana kwenye eneo la hatari la Tusker. Ni dhahiri shahiri upepo wa mashambulizi ya Al Ahly utakuwa mkali zaidi kwenye marudiano.
Ingawa katika kandanda lolote linaweza kutokea bado kibarua cha Tusker ni kigumu kupita maelezo.Vijana wa Kocha Robert Matano watahitaji kujitoa kwa mioyo yao yote,kucheza kwa roho za chuma na umakini wa fundi saa kupata matokeo ya kuridhisha mbele ya wajukuu wa Firauni.Historia inawahukumu vibaya Tusker,wakiitazama historia ya vilabu vya Kenya nchini Misri wanaweza kujiona panzi na kukata tama kabisa.Itawabidi kutoisoma historia au kuisahau kwa kuwa ishawapa hukumu ya kifo hata kabla ya mechi kuchezewa.Historia haichezi mpira,inaandikwa tu na walio shupavu na jasiri,hodari na makini.

No comments:

Post a Comment