Twitter

Twitter Buttons

Saturday 5 October 2013

Upofu wa Simba na Yanga, Ufanisi Uwanjani na Tuzo za Wanasoka Bora Tanzania

Japo tunahitaji kuwatuza wanamichezo wetu wanapofanya vizuri lakini bado sharti tuzo ziendane na vigezo stahili. Vigezo stahili ni vile vinavyo zingatia uwezo uwanjani, hatuhitaji vitu vya nje ya uwanja kuwa chachu ya kuwatuza wanamichezo Tanzania. Kwa nini tunashindwa kujifunza kwa waingereza tunaoshinda tukisema wanapiga 'kelele' licha ya kuwa wanapiga 'kelele' katika visiwa vyao na hawajatulazimisha kusoma magazeti yao na kuangalia mpira wao? Waingereza licha ya 'kelele' zao wanajali uvujaji jasho na shughuli ya mchezaji katika ugawaji wa tuzo zao, hawaangalii sana uzawa au uzalendo.Si ajabu kwa wageni kuchukua tuzo ya mwanasoka bora Uingereza kwa misimu mfululizo.

Hapa kwetu kuna tuzo mbalimbali lakini nyingi zimekuwa zikibagua wageni kwa misingi kuwa ni maalum kwa wanamichezo wazawa tu. Kuleta hoja ya utanzania kwenye michezo ni kuendeleza siasa kwenye mpira. Kwa nini mabao ya Kipre Tchetche yasimpe tuzo? Kwa nini uraia wake umtenge kwenye tuzo za wanasoka bora? Kwa nini tusiache ufanisi na utendaji uamue ugawaji wa tuzo uwanjani?

Tuzo za TASWA na tuzo nyingine zilizolenga promosheni za kibiashara zaidi zote zimeingia kwenye mkumbo wa kurusha jicho kwa Simba na Yanga tu. Mchezaji wa Kigeni anafunga mabao kumi nane lakini kwenye tuzo hayupo,mzawa anazifunga Simba na Yanga mabao mawili, anaingizwa kwenye orodha ya wanasoka bora...kweli tutafika? Ni rahisi kutamka kuwa hizi sio tuzo ni promosheni tu. 

Hivi inatusaidia nini tunapoamua kumpa tuzo ya mchezaji bora Kelvin Yondani na kumtenga Kipre Tchetche, Inasaidiaje kukuza mpira wetu? Bila kwenda mbali sana, jirani zetu wakenya licha ya kuwa na hisia kali za uzalendo labda kuliko sisi bado walimpa tuzo ya mchezaji bora mganda Danny Sserenkuma, ,mbona sisi tunaleta siasa kwenye mpira? Nani ana ujasiri wa kusimama na kutamka alimuona Themi Felix wa Kagera Sugar kwenye mechi zaidi ya nne kiasi cha kumweka mbele ya Didier Kavumbagu? Si kwamba Themi Felix aligonga vichwa vya habari kwa kuzifunga Simba na Yanga ndio maana anawekwa kwenye orodha?

Hivi akija mgeni wa soka la bongo asiyejua siasa za mpira wetu unawezaje kumuelezea kwa takwimu kwa nini Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche hawamo kwenye orodha ya wanaowania uchezaji bora huku Yondani, Themi Felix, Kapombe na Niyonzima wakiwepo? Kwa nini uwezo uwanjani usiwe kigezo kikuu bila kuleta uzawa na siasa kwenye tuzo. 

Kama si kutafuta kura za mashabiki wa Simba na Yanga kufanikisha promosheni utaelezeaje Kiemba kuwemo kwenye orodha huku Tchetche akikosekana? Hizi tuzo zinaangalia uwezo kwenye ligi kuu ama timu ya taifa au vyote, tunatofautishaje vitu hivi? Kama ni ligi kuu, Kiwango alichokionesha Kiemba akiwa Simba kwa vigezo vipi kimezidi kiwango cha Tchetche na Kavumbagu? Kama unaangalia na timu ya Taifa, mbona Niyonzima anajumlishwa licha ya kuwa hakuna lolote alilofanya timu yake ya Taifa?Kapombe alifanya kipi Simba ambacho Mbuyu Twite hakufanya ? Au ni lazima Simba ikitoa wachezaji wawili basi ili kuondoa kelele za Jangwani basi ni sharti Yanga nayo itoe wawili ili tuweze kuandika vichwa vya habari ' Simba na Yanga zatawala Tuzo' ?

Tuzo zetu ni muendelezo wa upofu wetu kwa Simba na Yanga. Tusipoandika Simba na Yanga gazeti haliuziki. TFF nao wanatangaza mapato ya mechi za Simba na Yanga tu. Waamuzi wanafungiwa kwa kuboronga mechi za Simba na Yanga tu. Tovuti ya ligi kuu inaweka takwimu kamili za mechi za Simba na Yanga tu. Kupata vikosi vya timu nyingine ni mpaka zicheze dhidi ya Simba na Yanga tu. Wadhamini wa ligi kuu wanatoa 'updates' kwa mechi za Simba na Yanga tu.

No comments:

Post a Comment