Twitter

Twitter Buttons

Thursday 31 October 2013

NI Wakati Wa Jeshi Kusema Yatosha Kwa Vipigo Wanavyopokea

Mbeya City wakishangilia goli la kwanza
Wakishangilia bao la pili (Picha zote za Mbeyayetu blog_











                        
Mashabiki wa Mbeya City waliamua kubeba jeneza na kulizungusha uwanjani kama ishara ya kuizika rasmi Tanzania Prisons baada ya kuiangushia kipigo cha mabao mawili kwa sifuri. Mpira ni burudani, na hii ilikuwa mojawapo ya burudani za mashabiki wa Mbeya City. Lakini ukiangalia kwa undani unaona hili ya kubeba jeneza ni utani uliobeba ujumbe wa ukweli ndani yake. Ukiwa na kichwa kikubwa kisha mtani wako akakutania kwa kukuita ‘bichwa’ utauchukulia kama ni ukweli au utani au vyote, yaani ni utani japo ni ukweli?

Prisons kubebewa jeneza na timu iliyopanda daraja msimu huu utabaki kuwa utani lakini kuna haja ya jeshi kutambua kuwa licha ya kuwa ni utani kuna ukweli ndani yake.  Ishara ya kubebewa jeneza kwenda kuzikwa iliendana na matokeo ya uwanjani na kuendeleza wimbi la matokeo mabovu kwa timu za jeshi msimu huu na msimu uliopita. 

Timu za jeshi zinapumulia mkiani kwenye msimamo wa ligi huku tatu zikivuta mkia kwa kufuatana kama mnyororo wa baiskeli. Prisons, Mgambo na Oljoro zimeambulia ushindi kwenye mechi moja moja tu kati ya kumi na moja zilizocheza mpaka sasa. Yaani hali ni mbaya kiasi kwamba ukichukua alama za Prisons, Mgambo na Oljoro jumla yake bado ni alama tatu pungufu kwa alama za Azam na Mbeya City. Jumla ya alama za timu hizi tatu za majeshi hazitoshi hata kuzipa nafasi ya nne. Ukijumlisha  alama zao zote Pamoja na mabao ya kufunga ukasema iwe timu moja basi kwa msimamo wa sasa timu hiyo itaangukia nafasi ya tano.

Prisons wanathibitisha ile hadithi ya askari magereza naye ni mfungwa tu kwa jinsi wanavyofungwa mechi baada ya mechi. Hawa maafande wa magereza wamegeuzwa wafungwa kwa kufungwa mechi tano kati ya 11 walizocheza hadi sasa. Hadi wana halmashauri wa Mbeya City wamewageuza ngazi ya kukwea kileleni na kuwadhihaki kwa kutembeza jeneza kama ishara ya mazishi yao.

Kwa upande wa pili ukiwaangalia Mgambo Shooting jinsi wanavyorukaruka na kuchanganyana uwanjani unaweza kuhisi Juma Nature alikuwa akiwatazama wakati anaandika mashairi  ya wimbo wake wa ‘ Mgambo’. Jezi zao za pundamilia, rangi nyeusi na nyeupe, mara moja zinakukumbusha zile filamu za makala za pundamilia wanavyoliwa na mamba wakati wa kuvuka mto Mara kati ya Tanzania na Kenya . Safu yao ya ulinzi inavuja kuliko nyumba  za nyasi  zilizochoka wakiruhusu mabao 21 kwenye mechi 11 na kuongoza kwa ukarimu. 

Amissi Tambwe wa Simba anaongoza ufungaji wa mabao (amefikiwa na Hamisi Kiiza wa Yanga) kwa sababu ya ukarimu wa safu ya Ulinzi ya Mgambo. Mabao manne ya Tambwe dhidi ya Mgambo yananikumbusha tena zile filamu za makala za mamba wanaofaidika na mlo wa bure kutoka kwa pundamilia na nyumbu wanaovuka Masai Mara kiasi cha kubaki na hifadhi ya msimu ujao kwa kula kidogo kidogo tu ile mizoga. Ni hadithi sawa na ya Tambwe, aliwapiga Mgambo bao nne kisha akaanza kujazilizia kidogo kidogo na bado anaongoza msimamo wa ufungaji. Mgambo Shooting walikuwa kama pundamilia kwake ilhali yeye akigeuka wale mamba wa Mto Mara.

Safu ya yao ya ushambuliaji ni kama ipo kwenye mgomo baridi kwa kufunga mabao matatu tu kwenye michezo kumi na moja! Bila shaka washambuliaji wake hawajui waliposahau viatu vyao vya ufungaji. Kwa hakika Mgambo wanazidi kulishusha hadhi jina la Mgambo ambalo tayari si kati ya majina yanayoheshimika hasa huko mtaani. Badala ya kututhibitishia kuwa Mgambo nao wamo wanaonekana kututhibishia zile hadithi zetu za uswahilini kuhusu Mgambo.

JKT Oljoro nao hali ni mbaya wakizidi kuwa rojorojo kwa  kupokea vipigo mara sita katika mechi 11. Hali ni ile ile kwa Ruvu Stars ambao inaonekana nyota yao pekee ni ushindi katika mechi nne na vipigo saba katika mechi 11. Nini kinasababisha matokeo mabovu kwa timu za majeshi? Mbona timu za majeshi zinafanya vizuri kwenye nchi nyingine? Rwanda kuna APR ambayo panga pangua haikosi tatu bora, Kenya kuna Ulinzi, Zambia wana Green Buffaloes, Morocco wana FAS Rabat ambazo ubingwa wa ligi haukaki kwa miaka zaidi ya mitatu, nini kinasumbua timu zetu za majeshi?



No comments:

Post a Comment