Mbeya City wakishangilia goli la kwanza |
Wakishangilia bao la pili (Picha zote za Mbeyayetu blog_ |
Mashabiki wa Mbeya City waliamua kubeba jeneza na
kulizungusha uwanjani kama ishara ya kuizika rasmi Tanzania Prisons baada ya
kuiangushia kipigo cha mabao mawili kwa sifuri. Mpira ni burudani, na hii
ilikuwa mojawapo ya burudani za mashabiki wa Mbeya City. Lakini ukiangalia kwa
undani unaona hili ya kubeba jeneza ni utani uliobeba ujumbe wa ukweli ndani
yake. Ukiwa na kichwa kikubwa kisha mtani wako akakutania kwa kukuita ‘bichwa’
utauchukulia kama ni ukweli au utani au vyote, yaani ni utani japo ni ukweli?
Prisons kubebewa jeneza na timu iliyopanda daraja msimu huu utabaki
kuwa utani lakini kuna haja ya jeshi kutambua kuwa licha ya kuwa ni utani kuna
ukweli ndani yake. Ishara ya kubebewa
jeneza kwenda kuzikwa iliendana na matokeo ya uwanjani na kuendeleza wimbi la matokeo
mabovu kwa timu za jeshi msimu huu na msimu uliopita.
Timu za jeshi zinapumulia mkiani kwenye msimamo wa ligi huku
tatu zikivuta mkia kwa kufuatana kama mnyororo wa baiskeli. Prisons, Mgambo na
Oljoro zimeambulia ushindi kwenye mechi moja moja tu kati ya kumi na moja
zilizocheza mpaka sasa. Yaani hali ni mbaya kiasi kwamba ukichukua alama za Prisons,
Mgambo na Oljoro jumla yake bado ni alama tatu pungufu kwa alama za Azam na
Mbeya City. Jumla ya alama za timu hizi tatu za majeshi hazitoshi hata kuzipa
nafasi ya nne. Ukijumlisha alama zao zote
Pamoja na mabao ya kufunga ukasema iwe timu moja basi kwa msimamo wa sasa timu
hiyo itaangukia nafasi ya tano.
Prisons wanathibitisha ile hadithi ya askari magereza naye
ni mfungwa tu kwa jinsi wanavyofungwa mechi baada ya mechi. Hawa maafande wa
magereza wamegeuzwa wafungwa kwa kufungwa mechi tano kati ya 11 walizocheza
hadi sasa. Hadi wana halmashauri wa Mbeya City wamewageuza ngazi ya kukwea
kileleni na kuwadhihaki kwa kutembeza jeneza kama ishara ya mazishi yao.
Kwa upande wa pili ukiwaangalia Mgambo Shooting jinsi
wanavyorukaruka na kuchanganyana uwanjani unaweza kuhisi Juma Nature alikuwa
akiwatazama wakati anaandika mashairi ya
wimbo wake wa ‘ Mgambo’. Jezi zao za pundamilia, rangi nyeusi na nyeupe, mara
moja zinakukumbusha zile filamu za makala za pundamilia wanavyoliwa na mamba
wakati wa kuvuka mto Mara kati ya Tanzania na Kenya . Safu yao ya ulinzi
inavuja kuliko nyumba za nyasi zilizochoka wakiruhusu mabao 21 kwenye mechi
11 na kuongoza kwa ukarimu.
Amissi Tambwe wa Simba anaongoza ufungaji wa mabao (amefikiwa
na Hamisi Kiiza wa Yanga) kwa sababu ya ukarimu wa safu ya Ulinzi ya Mgambo. Mabao
manne ya Tambwe dhidi ya Mgambo yananikumbusha tena zile filamu za makala za
mamba wanaofaidika na mlo wa bure kutoka kwa pundamilia na nyumbu wanaovuka Masai
Mara kiasi cha kubaki na hifadhi ya msimu ujao kwa kula kidogo kidogo tu ile
mizoga. Ni hadithi sawa na ya Tambwe, aliwapiga Mgambo bao nne kisha akaanza
kujazilizia kidogo kidogo na bado anaongoza msimamo wa ufungaji. Mgambo
Shooting walikuwa kama pundamilia kwake ilhali yeye akigeuka wale mamba wa Mto
Mara.
Safu ya yao ya ushambuliaji ni kama ipo kwenye mgomo baridi
kwa kufunga mabao matatu tu kwenye michezo kumi na moja! Bila shaka washambuliaji
wake hawajui waliposahau viatu vyao vya ufungaji. Kwa hakika Mgambo wanazidi
kulishusha hadhi jina la Mgambo ambalo tayari si kati ya majina yanayoheshimika
hasa huko mtaani. Badala ya kututhibitishia kuwa Mgambo nao wamo wanaonekana
kututhibishia zile hadithi zetu za uswahilini kuhusu Mgambo.
JKT Oljoro nao hali ni mbaya wakizidi kuwa rojorojo kwa kupokea vipigo mara sita katika mechi 11.
Hali ni ile ile kwa Ruvu Stars ambao inaonekana nyota yao pekee ni ushindi
katika mechi nne na vipigo saba katika mechi 11. Nini kinasababisha matokeo
mabovu kwa timu za majeshi? Mbona timu za majeshi zinafanya vizuri kwenye nchi nyingine?
Rwanda kuna APR ambayo panga pangua haikosi tatu bora, Kenya kuna Ulinzi,
Zambia wana Green Buffaloes, Morocco wana FAS Rabat ambazo ubingwa wa ligi
haukaki kwa miaka zaidi ya mitatu, nini kinasumbua timu zetu za majeshi?