ZALI LA
MENTALI LINAWEZA KUTUANGUKIA TAIFA STARS
Ukichunguza vizuri
ratiba ya mechi za kuwania kufuzu kombe la dunia kwa bara la Afrika utabaini mambo mawili.Mosi,hatua ya makundi
ndiyo ngumu zaidi hasa kwa kuwa ni timu moja tu ndiyo itafuzu kwa kila kundi.Kuna makundi kumi yenye timu
nne.Hivyo basi timu kumi zitakazoongoza makundi yao zitafuzu kwa hatua ya
mtoano ili kupata timu tano
zitakazowakilisha bara la Afrika kwenye kombe la dunia huko Brazil.
Hatua ya makundi ndiyo ngumu zaidi,kila timu itatakiwa
kucheza mechi sita,tatu ugenini na tatu nyumbani. Kwa hesabu za haraka haraka
mshindi wa kundi ni lazima ashinde mechi zote za nyumbani na angalau kushinda
mechi moja au kutoa sare mbili ugenini.Kwa vyovote vile ushindi wa nyumbani ni
lazima.Sare yoyote ya nyumbani ni kifo hasa ukizingatia kuwa ni timu moja tu
ndiyo itakayofuzu kwa kila kundi. Tanzania tumeanza vyema kwa kuwafunga Gambia
nyumbani,hatuna budi kuwafunga Simba wa milima ya Atlas kutoka Morocco ili
kuendeleza ndoto zetu za kuisaka safari ya Brazil.
Pili,utababini kuwa hatua ya mwisho ni rahisi na imejaa
bahati hasa kwa timu changa kama Tanzania.Hatua ya pili ni mechi mbili tu
zinakuvusha hadi Brazil kula bata.Yaani unahitaji kuwa makini katika dakika 180
tu kuungana na wababe wengine Brazil. Ni rahisi kushinda nyumbani na kwenda
kutafuta matokeo ugenini.Kwa mtindo huu Cape Verde walifuzu AFCON mbele ya
wababe Cameroun. Cape Verde walimaliza biashara nyumbani kwa kushinda 2-0 kisha
wakaenda kujitoa mhanga ugenini na kufungwa 2-1 na hivyo kuwatoa
Cameroun.Zambia waliokuwa mabingwa watetezi almanusra wavuliwe ubingwa wao pale
Kampala kabla ya kuponea chupu chupu kwenye matuta.Mtoano ni kamari nzuri kwa
timu changa.Usishangae kuwaona vigogo Afrika wakizikosa fainali za kombe la
dunia kwa mara nyingine huku ‘watoto’
wakifuzu.
Kwenye kundi letu Ivory Coast ana nafasi kubwa ya kufuzu licha ya kuwa ni mapema sana
kutabiri. Ivory Coast wana silaha za kutosha kuziketeza timu nyumbani na
ugenini.Historia yao ya hivi karibuni katika mechi za kufuzu inaonesha kuwa
hawana shida kuzifunga timu ugenini. Kumbuka jinsi walivyowalambisha sakafu
Senegal nyumbani na ugenini bila shida. Hawa wamekamilika.Hawa ndio
tunaowahofia sana.
Morocco licha ya kushiriki kombe la Afrika huko Afrika
Kusini na pia kutufunga nyumbani na ugenini katika mechi za kufuzu hawaonekani
kuwa tishio sana.Morocco hawakuonesha lolote la kutisha huko Afrika
Kusini,walitoa sare mechi zote.Pia hatuhitaji kwenda mbali sana kupata mfano
kuwa wanafungika.Jirani zetu wa Rwanda waliwakimbiza sana na kuwapakata kwa
kuwafunga 3-1 pale Kigali. Morocco pia wanaonekana kuwa na migogoro yao
kuhusiana na wachezaji wao nyota.Kina Adel Taarabt, Chamakh na Hamdaoui wa
Italia hawapo kwenye timu ya taifa kwa sasa.Kifupi hawa jamaa wanafungika.Pia
sare pale Rabat au Casablanca inapatikana tukiwa makini.
Gambia hao licha ya kuwa Afrika Magharibi si timu ya
kutisha,tuko katika kiwango
kimoja.Tumeshawafunga hapa,tunao uwezo wa kutoa nao sare au hata
kuwafunga huko kwao.Kifupi kama tukiwa
makini tuna uhakika wa point inane bila kuweka mechi ya Ivory Coast.Kwa hivyo
ni kuwa makini huku tukiomba Ivory Coast wajichanganye wenyewe.Kuteleza kwa
Ivory Coast ndiyo zali letu la mentali.Kumbuka Ivory Coast wenye kawaida ya
kushinda mechi zote wameisha toa sare moja,tumuombe Mungu waongoze sare
nyingine na Gambia.Dua zetu japo ni za kuku zinaweza kuwapata…Soka halichezewi
kanisani wala msikitini kwa hio maombi pembeni,maandalizi na mipango zaidi ili
zali la mentali liwe ukweli na si wimbo tu wa Profesa Jay.