Twitter

Twitter Buttons

Tuesday 31 December 2013

Hadhi ya Ernie Brandts, shoka la Manji na Sarakasi za Soka Bongo

Wahanga wa Panga la Manji: Tom Saintfiet na Ernie Brandts  


                
Hatimaye na kocha  Ernie Brandts naye ameonekana hafai, mzigo kwa klabu kubwa nchini. Kama ilivyo wengi waliomtangulia naye ameonekana uwezo wake umefikia kikomo. Mbinu zake zimewakinai wale walioahidi ujenzi wa uwanja kuanza miezi  sita iliyopita.
Wamempima kocha wakaona hawafai. Wamemtathmini na kutoa hukumu lakini kwa makusudi au la, wamesahau kujitathmini. Wamesahau kutathmini uzito wa ahadi zao na utupu wa utekelezaji wao mpaka sasa .
‘Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na wapinzani wetu, na soka tulilocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki kwa kweli ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.’ Hapa inaonekana kabisa Abdallah Bin Kleib naye ameanza kuamini ‘majina’ ya kwenye magazeti ya wachezaji wetu. Kumbe majina ya kuuzia magazeti yanasumbua hadi viongozi!
Sijui anaongelea uwezo upi wa mchezaji mmoja wakati tunavijua viwango vya wachezaji wetu. Kama ni viwango vya kwenye magazeti yetu basi ni sawa. Kiuhalisia wachezaji wetu wengi hawapishani sana uwezo na ndio maana unaangalia Yanga, Simba na Azam wakihema kupata ushindi dhidi ya akina pangu pakavu tia mchuzi, kina JKT Ruvu, Ashanti na wengineo.
Ligi inaisha, bingwa anapatikana lakini hakuna mchezaji anayefuzu majaribio hata Afrika Kusini.Si Yule nyota anayetawala vichwa vya habari wale yule mchezaji wa timu za jeshi anayejituma ili aonekane na Simba, Yanga na Azam.

Haingii akilini kusema kocha wa kiwango cha Ernie Brandts ameishiwa mbinu na hana njia mbadala ilhali uongozi uliopo umeshindwa kuonesha mbinu mbadala za kuingizia klabu mapato. Huu ujasiri unatoka wapi…ni komedi tamu!

Katika nchi za Afrika Mashariki hakuna shaka kuwa vilabu vya Tanzania vimepata bahati ya kufundishwa na makocha wa kigeni mara nyingi zaidi kuliko wenzetu. Kwa undani zaidi, hii si bahati iliyokuja kama ajali. Ni udhibitisho wa hamasa kubwa ya kamdanda nchini.Hamasa tunayoshindwa kuitumia ipasavyo.

Kati ya makocha wengi waliopata fursa ya kufundisha mpira Tanzania hasa katika muongo uliopita, mholanzi Ernie Brandts anaweza kuwa ndiye mwenye hadhi kubwa zaidi. Brandts si tu ni kocha wa kutoka nchi yenye hadhi ya juu kisoka, Uholanzi bali ni kocha aliyethibitisha uwezo wake kama mchezaji.

Brandts aliichezea klabu kubwa ya kwao, PSV kwa takriban muongo mzima. Alivaa jezi za timu ya taifa zaidi ya mara ishirini ikiwemo kushiriki katika kombe la dunia. Hakuwa tu mshiriki wa kombe la dunia, alibahatika kujiandika historia ya kuwa mfungaji wa mabao mawili. Alijifunga bao moja pale alipojikuta akiutumbukiza mpira  kwenye nyavu zao katika harakati za kuutoa mpira miguuni mwa mshambuliaji wa Italia. Katika historia ya pekee, aliisawazishia Uholanzi kwa shuti kali la mbali na kujiandikia historia ya pekee kwenye kombe la dunia.

Kama haitoshi, Ernie Brandts amefanya kazi na makocha maarufu duniani. Amepata bahati ya kuwa msaidizi wa Sir Bobby Robson, kocha wa zamani wa Barcelona na Newcastle, Dick Advocaat , kocha wa zamani wa timu za mataifa ya Uholanzi, Korea kusini na Urussi. 

Sababu  rasmi za kutimuliwa  kwake kwa mujibu wa tovuti rasmi ya klabu ni  ‘Maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.’ 

Hivi ni maana ya mwenendo mbaya? Timu iliyotwaa ubingwa miezi saba iliyopita na bado imemaliza ngwe ya kwanza ikiwa kileleni inakuwaje na mwenendo mbaya? Mwenendo upi mbaya ilhali timu haijafungwa kwenye mechi nane mfululizo za mashindano? Brandts ameiongoza Yanga kwenye mechi zaidi ya 35 na kupoteza mechi takriban nne tu ukijumlisha na za kirafiki pamoja na  ile ya ‘bonanza’ dhidi ya Simba.

‘Mwisho tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki…’ Mwanzoni tunaambiwa matokeo ya mechi ya Mtani Jembe ni moja ya sababu ya kutimuliwa kwa kocha, mwishoni tunaambiwa hio ilikuwa ni mechi ya bonanza au fete! Kocha anafukuzwa kwa matokeo ya mechi ya bonanza?

Inawezakana kuwa kuna mengi hatuambiwi kwenye sakata hili. Hata habari za chini ya kapeti nazo hazina kichwa wala masikio zaidi ya kuacha maswali yasiyo na majibu. 

Inawezakana kabisa uhusiano wa Yanga na Brandts ulikwisha vurugika kiasi kwamba talaka pekee ndio suluhisho. Ila hivi visingizio vya kuwa kocha kaishiwa mbinu ni kumshushia hadhi kocha na pia viongozi wenyewe kujipaka matope bila sababu ya msingi. 
 

No comments:

Post a Comment