Wahanga wa Panga la Manji: Tom Saintfiet na Ernie Brandts |
Hatimaye na kocha Ernie Brandts naye ameonekana hafai, mzigo kwa
klabu kubwa nchini. Kama ilivyo wengi waliomtangulia naye ameonekana uwezo wake
umefikia kikomo. Mbinu zake zimewakinai wale walioahidi ujenzi wa uwanja kuanza
miezi sita iliyopita.
Wamempima kocha wakaona hawafai. Wamemtathmini na kutoa
hukumu lakini kwa makusudi au la, wamesahau kujitathmini. Wamesahau kutathmini
uzito wa ahadi zao na utupu wa utekelezaji wao mpaka sasa .
‘Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na
wapinzani wetu, na soka tulilocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki kwa
kweli ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.’ Hapa
inaonekana kabisa Abdallah Bin Kleib naye ameanza kuamini ‘majina’ ya kwenye
magazeti ya wachezaji wetu. Kumbe majina ya kuuzia magazeti yanasumbua hadi
viongozi!
Sijui anaongelea uwezo upi wa mchezaji mmoja wakati
tunavijua viwango vya wachezaji wetu. Kama ni viwango vya kwenye magazeti yetu
basi ni sawa. Kiuhalisia wachezaji wetu wengi hawapishani sana uwezo na ndio
maana unaangalia Yanga, Simba na Azam wakihema kupata ushindi dhidi ya akina
pangu pakavu tia mchuzi, kina JKT Ruvu, Ashanti na wengineo.
Ligi inaisha, bingwa anapatikana lakini hakuna mchezaji
anayefuzu majaribio hata Afrika Kusini.Si Yule nyota anayetawala vichwa vya
habari wale yule mchezaji wa timu za jeshi anayejituma ili aonekane na Simba,
Yanga na Azam.
Haingii akilini kusema kocha wa kiwango cha Ernie Brandts
ameishiwa mbinu na hana njia mbadala ilhali uongozi uliopo umeshindwa kuonesha
mbinu mbadala za kuingizia klabu mapato. Huu ujasiri unatoka wapi…ni komedi
tamu!
Katika nchi za Afrika Mashariki hakuna shaka kuwa vilabu vya
Tanzania vimepata bahati ya kufundishwa na makocha wa kigeni mara nyingi zaidi
kuliko wenzetu. Kwa undani zaidi, hii si bahati iliyokuja
kama ajali. Ni udhibitisho wa hamasa kubwa ya kamdanda nchini.Hamasa tunayoshindwa kuitumia ipasavyo.
Kati ya makocha wengi waliopata fursa ya kufundisha mpira
Tanzania hasa katika muongo uliopita, mholanzi Ernie Brandts anaweza kuwa ndiye
mwenye hadhi kubwa zaidi. Brandts si tu ni kocha wa kutoka nchi yenye hadhi ya
juu kisoka, Uholanzi bali ni kocha aliyethibitisha uwezo wake kama mchezaji.
Brandts aliichezea klabu kubwa ya kwao, PSV kwa takriban
muongo mzima. Alivaa jezi za timu ya taifa zaidi ya mara ishirini ikiwemo
kushiriki katika kombe la dunia. Hakuwa tu mshiriki wa kombe la dunia,
alibahatika kujiandika historia ya kuwa mfungaji wa mabao mawili. Alijifunga
bao moja pale alipojikuta akiutumbukiza mpira
kwenye nyavu zao katika harakati za kuutoa mpira miguuni mwa
mshambuliaji wa Italia. Katika historia ya pekee, aliisawazishia Uholanzi kwa
shuti kali la mbali na kujiandikia historia ya pekee kwenye kombe la dunia.
Kama haitoshi, Ernie Brandts amefanya kazi na makocha
maarufu duniani. Amepata bahati ya kuwa msaidizi wa Sir Bobby Robson, kocha wa
zamani wa Barcelona na Newcastle, Dick Advocaat , kocha wa zamani wa timu za mataifa
ya Uholanzi, Korea kusini na Urussi.
Sababu rasmi za
kutimuliwa kwake kwa mujibu wa tovuti
rasmi ya klabu ni ‘Maamuzi hayo
yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu,
kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.’
Hivi ni maana ya mwenendo mbaya? Timu iliyotwaa ubingwa
miezi saba iliyopita na bado imemaliza ngwe ya kwanza ikiwa kileleni inakuwaje
na mwenendo mbaya? Mwenendo upi mbaya ilhali timu haijafungwa kwenye mechi nane
mfululizo za mashindano? Brandts ameiongoza Yanga kwenye mechi zaidi ya 35 na
kupoteza mechi takriban nne tu ukijumlisha na za kirafiki pamoja na ile ya ‘bonanza’ dhidi ya Simba.
‘Mwisho tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa Yanga
wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki…’ Mwanzoni
tunaambiwa matokeo ya mechi ya Mtani Jembe ni moja ya sababu ya kutimuliwa kwa
kocha, mwishoni tunaambiwa hio ilikuwa ni mechi ya bonanza au fete! Kocha
anafukuzwa kwa matokeo ya mechi ya bonanza?
Inawezakana kuwa kuna mengi hatuambiwi kwenye sakata hili. Hata
habari za chini ya kapeti nazo hazina kichwa wala masikio zaidi ya kuacha maswali
yasiyo na majibu.
Inawezakana kabisa uhusiano wa Yanga na Brandts ulikwisha
vurugika kiasi kwamba talaka pekee ndio suluhisho. Ila hivi visingizio vya kuwa
kocha kaishiwa mbinu ni kumshushia hadhi kocha na pia viongozi wenyewe kujipaka
matope bila sababu ya msingi.